Sababu za Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa AFCON 2027

AJIRA MPYA ZA WIKI HII BONYEZA HAPA
AUDIOS MPYA ZA WIKI BONYEZA HAPA
VIDEOS MPYA ZA WIKI HII BONYEZA HAPA


Sababu za Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa AFCON 2027

Sababu za Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa AFCON 2027
Tanzania, Kenya na Uganda zimeingia rasmi kwenye mchakato wa kuwania kuwa wenyeji wa michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (African Cup of Nations) ya mwaka 2027.
Nchi hizi zinataka kuandaa kwa pamoja Fainali za 36 za AFCON 2027 kupitia mpango wao waliouita ‘Pamoja Bid’.
Kama zitafanikiwa kuwa wenyeji itakuwa rekodi ya kihistoria kwa kuwa itakuwa ni kwa mara ya kwanza Mashindano hayo kufanyika katika Ukanda wa Afrika Mashariki tangu yalipoanzishwa rasmi mwaka 1957.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania Jumatano ya Mei 24, 2023 alipokea andiko maalumu la ombi la Tanzania, Kenya na Uganda kuwa mweyeji wa AFCON 2027 kutoka kwa Rais wa Shirikisho la soka Tanzania, TFF, Wallace Karia.

Rais Samia Suluhu wa Tanzania akipokea andiko la Pamoja Bid kutoka kwa Rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, Mei 24, 2023.
Mwenzake wa Kenya, William Ruto alipokea andiko la aina hiyo Mei 15, 2023 huko Ikulu ya Nairobi kutoka kwa viongozi wa shirikisho, FKF chini ya Rais Nick Mwendwa.
Na kwa Uganda, Naibu Spika wa Bunge, Thomas Tayebwa, Waziri wa nchi Peter Ogwang na bosi wa Shirikisho la mpira (FUFA), Moses Magogo waliongoza ujumbe uliowasilisha hati ya mpango huo kwa Rais Yoweri Museveni na Mke wake ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Michezo, Janet Museveni, huko Ikulu ya Entebbe.
Pamoja na dhamira njema ya mataifa hayo matatu ndugu kutaka kuandaa michuano hiyo kwa pamoja, kuna vigezo muhimu vya kuzingatiwa vinavyoongeza fursa na changamoto kadhaa kuhusu uwenyeji wao.

Rais William Ruto wa Kenya akizungumza mara baada ya kupokea andiko la ‘Pamoja Bid’. Ilikuwa Mei 15, Ikulu Nairobi.
Zifahamu Fursa za kuwa Mwenyeji wa mashindano
Iliwachukua Uganda miaka 38 kufuzu tena AFCON (2017), tangu wafanye hivyo mwaka 1978. Ndugu zao Tanzania iliwachukua miaka 39 kufuzu AFCON (2019) toka ifanye hivyo mwaka 1980.
Tangu yaanzishwe miaka 66 iliyopita, Kenya yenyewe imewahi kufuzu mara 6 na kwa mara ya kwanza ilifuzu mwaka 1972. Tanzania imewahi kushiriki mara mbili tu fainali za AFCON (1980 na 2019) na Uganda yenyewe imeshiriki AFCON mara 7 kwa mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1962.
Kwa hivyo fursa ya kwanza ya wazi kabisa kwa nchi hizi ambazo hufuzu kwa shida Mashindano hayo, ni kuingia ama Kufuzu moja kwa moja kuchezwa fainali za AFCON 2027.
Ukiachana na kutangaza Utamaduni na kuongezeka kwa shughuli za kijamii, fursa ya pili kubwa ni ya kiuchumi.
Mashindano yaliyopita ya AFCON 2019 yaliyofanyika nchini Misri baada ya kushindikana kufanyika Cameroon kwa sababu za kiusalama, yaliliingizia taifa hilo mapato yanayofikia dola $83 millioni.
Kiwango kama hicho kilipatikana yalipofanyika Guinea ya Ikweta mwaka 2015 na Gabon mwaka 2017.
Hamasa ya soka kwa nchi hizi ukiachana na Misri ni ya kawaida ukilinganisha na nchi kama Tanzania. Wastani wa mashabiki walioingia viwanjani kwa mechi za AFCON 2019 ni watu 18,000, kiwango ambacho kwa Tanzania ni cha kawaida hasa linapohusisha mechi kubwa.
Huenda isiwe sawa kwa majirani zake Uganda na Kenya, lakini Mashindano hayo yatavutia maelfu kwa maelfu ya

Sababu za Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa AFCON 2027
watu hata wasiofuatilia sana mpira.
Na hiki ndio hasa kinazisukuma nchi hizi tatu kutaka kuandaa AFCON 2027.
AFCON huvutia Mabilioni ya watu. Zaidi ya watu Bilioni 1 hutazama Mashindano haya kupitia Runinga. Hakuna asiyetaka kumuona mchezaji kama Achraf Hakimi wa Morocco, ambaye hivi karibuni alizua gumzo kwa kutompa chochote mtalaka wake, akiweka mali zake zote kwenye jina la mama yake. Mwaka 2027 atakuwa na miaka 28.
Huo utakuwa mwaka wa nyota kama Amad Diallo winga wa Manchester United kutoka Ivory Coast, Edmond Tapsoba mwenye umri wa miaka 22 wa Bayer Leverkusen kutoka Burkinafaso, Kreptin Diatta mwenye umri wa miaka 22 anayetajwa kuwa mchezaji bora kijana wa Afrika kwa sasa aliyejizolea sifa katika AFCON 2019 akiwa na Senegal na anayekipiga huko Ubelgiji na Club Brugge.
Wako wengi ambao macho ya Dunia yatakuwa yakiwatazama. Pape Matar Sarr kinda wa miaka 20 na mshindi mwingine wa AFCON akiwa na timu ya taifa ya Senegal anayechezea Tottenham Hotspurs.
Wengine ni David Fofana wa Chelsea na Ivory Coast, Tariq Lamptey (Ghana), Cheick Doucouré (Mali), Rayan Aït-Nouri (Algeria) na Samuel Chukwueze (Nigeria).
Sijawataja Mohammed Salisu wa Ghana na Southampton, Kelechi Iheanacho wa Nigeria na Leicester atakeyekuwa na miaka 30, kama ilivyo kwa Gnaly Cornet wa Westham na Ivory Coast.
Ukiacha shughuli za kijamii kuongezeka wakati wa mashindano, AFCON ni fursa nzuri ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ukanda huu na vitakavyoleta wageni kwa miaka 10 mpaka 20 ijayo.
Atakavyokuja Hakimi na timu yake ya taifa, atapata fursa ya kujua vivutio vya Utalii, atakaporejea kwenye timu yake ya PSG huko Ufaransa, haitakuwa kitu cha ajabu akimsimulia rafiki yake Kylian Mbappe, na hapo lengo la kutangaza utalii kupitia soka linajionesha, na Mbappe akija kutembelea vivutio Afika Mashariki ama watu wengine wanaomzunguka, lengo linakuwa limetimia.
‘Mapato ya Mashindano haya si ya viingilio tu, bali ni kuiweka nchi kweye ramani, hivyo utakuza utalii, utajenga ajira utainua kipato, miundombinu itaimarishwa, biashara zitaongezeka na hapo ndipo unaponufaika kiuchumi kupitia aina hii ya mashindano’, anasema Juma Shomvi, mchambuzi na mfuatiliaji wa soka Tanzania.
Vigezo vya kuandaa AFCON na changamoto kwa Tanzania, Kenya na Uganda
Moja ya vitu vikubwa wanavyoviangalia CAF wanapotaka kuipa uenyeji wa AFCON nchi fulani ni pamoja na kuwa na viwanja vizuri vinavyokidhi vigezo, angalau viwanja 6 kwa nchi inayoandaa peke yake ama viwanja 8 kwa nchi zinazoandaa kwa pamoja.
Kati ya viwanja hivyo angalu viwili viwezo kuchukua watu angalau 40,000, viwili vingine angalau 20,000 na vingine angalau viwe na uwezo wa kuingiza watazamaji 15,000.
Hoteli nzuri kwaajili ya malazi ya wachezaji, benchi la ufundi, maafisa na wageni wengine, viwanja vya mazoezi, usafiri wa uhakika pamoja na suala la usalama linalozingatiwa sana.
Kwenye mahoteli, viwanja vya mazoezi au usafiri huko hakuna tatizo sana, nchi hizi zinaweza kukidhi kirahisi lakini maeneo mawili yanayoweza kuwa kikwazo ni miundo mbinu ya viwanja na usalama hasa kwa Kenya.

Kushoto ni Uwanja wa Taifa nchini Tanzania (Benjamini Mkapa) na Uwanja wa taifa wa zamani ambao sasa umesalia kuitwa Uwanja wa Uhuru
Baada ya uchaguzi wa Agosti 2022, hakuna mwenye uhakika kwamba hakutakua na ghasia za maandamano kesho. Lakini uchaguzi ujao wa 2027 hakuna mwenye uhakika usalama wake utakuwaje.
Tanzania usalama si tatizo sana, kwa Uganda usalama ni suala mtambuka. Mwaka 2017 Libya ilipokonywa uenyeji wa AFCON kwa sababu za kiusalama.
‘Usalama ni kigezo muhimu, Kenya wana muda wa kurekebisha hili ingawa hali sasa imetulia, na huwezi ifananisha na ile ya mwaka 2007 iliyoua karibu watu 1,000, ikiwa hivi mpaka mwaka 2027 haitakuwa tatizo’, anasema Seif Shangali, mchambuzi wa soka Tanzania.
Kwenye eneo la miundo mbinu, mpaka sasa Kenya wana kiwanja kimoja tu cha Nyayo (30,000) kilichopo Nairobi kilichokidhi vigezo vya CAF kuchezea michezo ya kimataifa.
Uwanja wa Kasarani wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 60,000 pia unaweza kufikia vigezo hivyo ukiendelea na ukarabati.
Mwaka 2018 Kenya iliondolewa kuwa mwenyeji wa mashindano ya CHAN miezi minne kabla ya kuanza kwa mashindano hayo kwa sababu ya viwanja vyake kutokuwa tayari.

Uwanja wa Mandela, Uganda
Na CAF iko makini inapofika suala la viwanja, Guinea ilikuwa iandae mashindano ya AFCON 2025 lakini kutokana na maandalizi duni, Oktoba mwaka jana ikaiondoa haki hiyo na sasa haijatangaza mwenyeji wa mashindano ya mwaka huo.
Kwa Tanzania, inajivunia Uwanja wa Benjamini Mkapa, Uwanja wa Uhuru na Uwanja wa Amani Zanzibar kama marekebisho yatatakiwa hayawezi kuwa makubwa kiasi cha kutiliwa shaka uwezo wake, lakini ina mpango wa kujenga uwanja mkubwa wa kisasa mjini Dodoma. Je utakamilika kabla ya mwaka 2027? Hili ni suala la kusubiri.
Hiyo itakuwa sehemu ya bilioni 200 zilizotengwa kwaajili ya kuboresha miundo mbinu ya michezo nchini ikiwemo kujenga Arena ya kisasa ya michezo na sanaa katika eneo la Tanganyika Packers, Kawe.
Licha ya kuwa na viwanja vyenye majina Afrika Mashariki vya Nakivubo (30,000), uwanja mkongwe zaidi Uganda, Amahoro (30,000) na Mandela (45,000), kwa sasa Uganda yenyewe haina uwanja hata mmoja uliokidhi vigezo vya kuchezea mechi za kimataifa na hilo limeifanya hata timu ya taifa ya the Uganda Cranes kucheza na Tanzania kwenye ardhi ya Misri wakati wa mchezo wa kufuzu kwa fainali za mwaka huu za AFCON. Uwanja wa Mandela uko hoi ukiendelea kukarabatiwa.
Hii ni mipango ya mataifa haya ili kutimiza ndoto ya uenyeji AFCON 2027
Inaonekana nchi hizi zimepania kweli kweli. Serikali imekuwa mshirika mkubwa kusaidiana na mashirikisho ya soka kutimiza ndoto hii.
Ushahidi ni namna marais wa nchi zote walivyokuwa ‘bize’ mwezi huu kupokea andiko la ‘Pamoja bid’ kuonesha mpango huo na nini vinavyohitajika.
Kazi kubwa ya Kenya ni kuhakikisha angalau viwanja vitatu vinafikia vigezo vinavyohitajika kama ilivyo kwa Uganda na Tanzania, lakini itahitaji kushughulikia suala la usalama.
Tanzania yenyewe ilishaweka mipango yake wazi, ikiwemo kujenga uwanja mwingine wa kisasa utakaoingiza watu 60,000 pale Dodoma lakini wanaweza kurekebisha uwanja mwingine mkubwa wa CCM Kirumba uliopo Jijini Mwanza.
‘Mheshimiwa rais anakwenda kujenga uwanja wa kisasa kabisa pale Dodoma, pengine utafanafana na uwanja wa Emirates (wa Arsenal). Lakini pia tuna viwanja saba ambavyo tunakwenda kuvikarabati na kuviboresha katika kiwango cha kimataifa, dhamira aliyonayo na ndoto aliyonayo rais wetu ni kuhakikisha kuwa kwa mwaka 2027, Tanzania tunakuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON kwa mwaka 2027’, ni kauli ya aliyekuwa Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo wa Tanzania, Mohammed Mchengerwa, aliyoitoa jijini Dar es Salaam..

Rais Yoweri Museveni akipokea andiko la ‘Pamoja Bid’ la kuandaa AFCON 2027 kutoka kwa Waziri wa Elimu na Michezo, Janet Museveni, ambaye ni mkewe, Mei 22, 2023.
Mataifa gani mengine yanayowania uenyeji wa AFCON 2027?
Nchi nyingine zilizoomba kuandaa AFCON ya 2027 ni Botswana, Algeria na Misri.
Ukizitazama vyema nchi hizi ni Misri na Algeria zinaweza kuwa tishio na kuzima ndoto za Tanzania, Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa AFCON 2027.
Misri imetoka kuandaa fainali za AFCON 2019 na Algeria yenyewe imetoka kuandaa mashindano dada ya AFCON ya wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika (CHAN 2023) yaliyofanyika mapema mwaka huu.
Kwa mantiki hiyo nchi hizi, hazitakuwa na matatizo ya miundo mbinu ya viwanja, viko tayari, wanavyo vya uhakika na vyenye hadhi na mahitaji mengine muhimu. Ziko kwenye nafasi nzuri zaidi ukilinganisha na za Afrika Mashariki.
Botswana ilikuwa iandae kwa pamoja na Namibia, lakini Namibia imejitoa dakika za mwisho kutokana na uhaba wa fedha.
Botswana si tishio sana na hawana viwanja vikubwa lakini mipango yao ya kuboresha na kujenga uwanja mkubwa unaweza kutishia uenyeji wa nchi za Afrika Mashariki.
Kwa sasa uwanja wao wa taifa uliopo Gaborone unaoingiza watu 25,000, Uwanja wa Francistown (27,000) na New Lobatse (20,000) vinatizamwa kusaidia harakati ya kupata uenyeji wa AFCON 2027.
CAF inatarajiwa kutangaza majina ya mataifa yaliyoomba kuandaa AFCON 2027 wakati wowote kabla ya kufanya ukaguzi wao kati ya Juni 1 mpaka 15, 2023.
Mwezi Septemba itatangaza mwenyeji wa AFCON 2027 ambaye atapewa miaka minne ya kujiandaa. Hivyo Tanzania, Kenya na Uganda kama zitafanikiwa kupata haki hiyo, hata kama zina mapungufu leo, zina nafasi ya kuyarekebisha ndani ya miaka minne ijayo.
Credit: BBC Swahili
PIA UNAWEZA KUSOMA👇
- Ada/makato ya Lipa kwa M-pesa, Lipa kwa Simu
- ADA za LIPA kwa Airtel Mitandao Yote
- TETESI za Usajili NBC Premier League 2023/2024
- YANGA yashika Nafasi ya 9 Simba ya 10 Afrika 2022/2023
- FAHAMU kuhusu Azam Pesa pamoja na Makato yake
- Ada mpya za M-Pesa 2023/2024 | Makato mapya ya M-Pesa
- Ada zaAirtel Money 2022/2023 | Makato mapya ya Airtel Money
- ADA Mpya za Tigo Pesa (Tigo Pesa Tariffs 2022/2023)
- Ada/Makato ya HaloPesa Tanzania, Halopesa Tariffs 2023
- DOWNLOAD | NYIMBO ZA TENZI ZA ROHONI SWAHILI MIX
- Ada za M-Pesa Songesha 2022/2023
- FAHAMU Jinsi ya Kufungua Akaunti ya M-Koba Vodacom
- Namna ya Kujisajili na Premier Bet Ushinde Mamilioni
- RATIBA kamili NBC Premier League msimu wa 2022/2023
- DOWNLOAD NIDA number | Kitambulisho cha Taifa
- MSIMAMO Ligi Kuu Tanzania Bara 2022/2023
- WAFUNGAJI Wanaoongoza kwa Ufungaji Ligi Kuu
Nijuze TV ni App ambayo ukiwa nayo utaweza kutazama mechi za Ligi Kuu Tz Bara (NBC PREMIER LEAGUE) EPL, WORLD CUP, EPL, LALIGA, SERIA, LIGUE 1, BUNDESLIGA na Ligi nyingine nyingi.
Download App ya Nijuze Habari Playstore tukutumie Habari zote kwenye Simu yako BILA MALIPO BOFYA HAPA.
Download App ya Nijuze TV Utazame mechi zote kwenye Simu yako BOFYA HAPA
Tags: Kenya na Uganda kuandaa AFCON 2027, Sababu za Tanzania